Bride Shoes

Bibi Harusi Mtarajiwa Mtajika

= 3092

Ama kweli wa kusema husema,kwangu mimi kama kuna jambo ambalo naishi nikiota usiku na mchana ni kufanya harusi.Nina ari ya kuvalia nguo nyeupe pe kama theluji,kutengeneza nywele zangu na kuvaa viatu vya visigino virefu huku nikijishaua kwa maringo na mwendo wa polepole kama bibi harusi.
Ili kuonyesha haja yangu ya kufanya harusi niliamua kuwaalika wageni katika harusi yangu ambayo itafanyika hivi karibuni.Mpenzi msomaji naomba tusome barua hii kwa pamoja.
BARUA YA MWALIKO WA HARUSI YANGU
KWA MASAHIBU,JAMMA NA MAADUI (YAANI WENYE VINYONGO),
Nina furaha riboribo kuwaalika katika harusi yangu itakayofanyika hivi karibuni.Itakuwa tarehe mosi,agosti mwaka ambao nitaposwa na mpenzi wangu ambaye kwa sasa sina.
Wahenga walinena kuwa msafiri ni aliye bandarini.Licha ya kuwa sijapata posa najianda katika harusi ya kufana.
Najipima nguo nitakayovalia siku ya harusi,viatu,kuandika bajeti ya siku hiyo na hata kufikiria ni nani kati ya rafiki zangu atakuwa bi harusi wangu au mama mlezi wangu katika harusi.
Harusi yenyewe itafanyika katika kanisa la mpenzi wangu huko kwao kijijini.Natarajia kuwa atakuwa mcha Mungu na atatoka kijijini.
Mnaombwa kufika siku hiyo bila kuchelewa.

Wenu mwaminifu,
Sahihi.
Bi harusi mtarajiwa mtajika.

Kila niskiapo watu wakinena kuwa kufanya harusi ni kupoteza pesa,mie hukereka sana.Kwa nini watu hawa wanakuwa wachoyo namna hii? Pesa ni maua hapa duniani.Tunapaswa kuzitumia ziishe zote ili tutafute zingine.Kwa sababu hii, nguo yangu ya harusi itaagizwa kutoka London.Nimejipima ya shoga wangu lakini ni ndogo mno.Amenielezea kuwa ni ya humu nchini.Jambo la kukera ni kuwa ni ya bei nafuu,kama bei ya kununua pipi.Nilishukuru Maulana kuwa gauni hilo la harusi halikunitosha.Nani avalie gauni la rejareja kama hilo?

Katika harusi yangu sitawahusisha katika mchango wa pesa za kununua hiki na kile.Watu wengi hasa jamaa,marafiki na maadui ni mkono birika.Wengi hukereka wakiombwa kuwa katika kamati andalizi ya harusi.Hawapendi kamwe kutoa hata senti moja.Habari njema ni kuwa sitahitaji hizo hela.

Mume wangu mtarajiwa ambaye mi humuota kila usiku ( mrefu kama jadi yetu na mwenye kifua kipana kama ardhi)nataraji atakuwa na hela za kutosha.
Nitafurahi kama kipofu aliyetahamaki anaona kutembea na mume wangu kanisani,kucheza naye baada ya harusi na hata kwenda fungate.

Harusi ni njia mojawapo ya mume kuonyesha kuwa kwa kweli anakuenzi kama mboni ya jicho lake.Anakubali kufungwa pingu ndogo kabisa ulimwenguni(pete)kwa sababu yako.Licha ya kuwa waume wengine ni viruka njia hata baada ya harusi,ni jambo la kufariji kujua kwamba iwapo mtatengana utapata nusu ya mali yake.Jambo hili lanifurahisha si haba.Eti mimi ni maskini hohe hahe au maskini wa kutupwa lakini kwa sababu nimefunga ndoa na mwanamme tajiri,nina kifurushi changu cha fedha iwapo tutatengana naye.
Ndoa pia humpa mtu hadhi ya juu katika jamii.Ningependa kuonyeshwa kuwa ni mimi niliyefanya harusi.

Ili kuhakikisha kuwa harusi yangu inafanaa ninafanya mazoezi ya hapa na pale ya namna ya kutembea na viatu vya visigino virefu.Sio eti mimi ni mshamba na nikiulizwa namna ya kutembea na viatu virefu siungami chochote.La,nimezoea kuvitoa kila mara nikichoshwa navyo.Kwa hivyo kama bibi harusi mtarajiwa mtajika napaswa kuwa mstaarabu.Sipaswi kuonekana ni kana kwamba navumilia kuvivalia viatu.Picha ikipigwa napaswa kutabasamu kwa furaha.Iwapo nimechoka kuvalia viatu virefu naweza kunja uso wangu kama mtu aliyekunywa maji kali ya ndimu.Hilo halitakuwa jambo la kufurahisha kamwe katika harusi.Kwa hivyo, nahakikisha kuwa kila jioni natembea huku na huko sebuleni kwa muda wa saa moja ili nimakinike na nistaarabike katika kutembea na viatu hivyo.

Jambo lingine la kufanikisha harusi ni kuhakikisha kuwa sihadaiki kuishi maisha ya paka na panya na mume yeyote. Mume wa aina hii hatakuwa radhi kufanya harusi.Atatoa ahadi tupu ambazo zaweza kunighadhabisha bure.Kwa hivyo bora kutahadhari kabla ya hatari.Mume ambaye ana hamu ya kuchovya asali na kuondoka hana nafasi karibu nami.Yeyote anayesema kuwa harusi ni kupoteza pesa,bila shaka hana budi kutoweka mbali na asionekane usoni mwangu tena.

Kama tujuavyo harusi ni sherehe yenye raha na matarajio ya maisha mazuri kwenye ndoa.Hata hivyyo, ndoa ni mtihani uliowashinda wengi hata maprofesa.Wakati mwingine ndoa huenda ikawa karaha kwa wengi.Hata hivyo kama bibi harusi mtarajiwa mtajika natumai kuwa ndoa yangu itakuwa ya kufaana kama harusi itakavyokuwa.
Sina mengi.Natumai kuwaona kwenye harusi yangu siku za usoni panapo majaliwa.

Use Facebook to Comment on this Post

Related Posts:

  • No Related Posts

About Agnes Sikuku

Check Also

Uchawi wa Mombasani

Post Views = 4120 Niliamka asubuhi mbichi kwa mshtuko ! Kufungua macho nikakaribiswa na magome …

SIMU YA KIFO

Post Views = 3563Ilikuwa jumamosi ya aina yake nikiwa kwenye mikiki mikiki ya wikendi. Matanuzi …

Leave a Reply

Connect with:
Your email address will not be published. Required fields are marked *