Uchawi wa Mombasani

= 4137

Niliamka asubuhi mbichi kwa mshtuko ! Kufungua macho nikakaribiswa na magome na majabali ya ufuo wa bahari. Nilikuwa uchi wa mnyama sawia na nilivyotoka tumboni mwa mamangu. Mng’aro wa jua ulikuwa ukiacha vimulimuli kwenye mawimbi mapevu ya bahiri Hindi. 

 

 

Hali ya mkanganyiko ilinifika. Maswali lukuki yalipishana ubongoni mwangu bila majibu, sikujua nianzie na wapi nimalize na wapi. Upweke ulikuwa umeumeza ufuo, hakukuwa na alama ya binadamu. Mawimbi ya bahari yalikuwa yakigonga miamba na kuacha sauti za kutisha zikihinikiza. Nilinyanyuka kwa unyonge nikasimama na kutazama kiwiliwili changu huku hofu ikinikula vilivyo.

 

 

Jambo kama hili halikuwa limenitukia kabla lilikuwa geni aushini mwangu japo mara nyingi husukia limewafika wengine hapa mjini Mombasa.  Nilikaa tutwe nikiwaza na kuwazua kama jana kuliendaje, fikra za vitushi na matukio ya kumbukumbu zikaanza kupiga makasia na kutiririka ubongoni.  Ajabu ilioje?

 

Nilitoka nyumbani kwangu siku iliyopita katika viunga vya mji wa Mombasa, Kisauni kuelekea kwenye Jomvu nilikokuwa nikifanya kijungu jiko. Kutoka tu nyumbani mwangu nivaana na paka mwuesi tititi, kwenda kumfukuza paka huyo alinitumbulia macho na akagoma kutoroka. Nilimuita bibi yangu ashuhudie maajabu haya. Paka yule alipigapiga mkia chini akatoa mlio wa ajabu kisha akatoweka. Sikuitilia maanani drama ya paka yule bali nilitoka nyumbani kuelekea kazini.

 

Nilivyokuwa kuwa nikitembea nilikumbuka siku moja nilipotoka kutazama kabumbu baina ya Man United na Arsenal nilifika kwangu saa saba usiku. Nilipofika kwangu nilishangaa kuona kitoto cha miaka kumi binti wa jirani yangu Kazungu kikiwa mlangoni  pangu. Cha ajabu mtoto yule alikuwa kajipaka makaa usoni na kavaa kama mganga, mikononi alikuwa ameshikilia vitu vya kichawi. Nilijaribu kumshika nimuulize maswali kadhaa ila alipaza sauti ya kutisha akisema, “nahenda kazi ma’ma”, (nafanya kazi ya mama) kisha akapotea kama upepo nisimwone tena machoni. Kutoka siku hiyo nilikuwa bubu hadi siku ya tatu nilipokuja ombewa na pasta wangu ndipo nikaweza kuongea tena.

Nilipofika kazini sikuwa na amani. Nilikuwa na mawazo mengi. Jioni ilipofika niliondoka guu mosi kuelekea kwangu. Nilikata mitaa ya Mwembe Tayari, Tudor,  Sabasaba, Lights hadi mtaa wa Bakarani nilikoishi. Bakarani ni mtaa wa wahuni, wezi na wabakaji. Ila hayo ni kidogo, maswala ya uchawi na ndumba yamekita mizizi kwenye mtaa huu. Ukitembea usiku wa manane ni rahisi kukutana na jini. Unaweza kuona mnyama akiwaka mataa, wachawi wakiwa uchi ama aina nyingine ya ushirikina.

Nilipotoka kazini sikuenda moja kwa moja bali nilipitia mangweni (klabu ya kienyeji) kupata chupa kadhaa za pombe ya  mnazi. Mangweni niliwakuta wazee kadhaa wakinywa huku wakipiga soga za kilevi.  Niliagiza chupa moja kutoka kwa mama mchuzi na nikaanza kuvuta polepole bila mshkili wowote.  Kabla hata sijafikisha pombe yangu katikati Mzee Kizingo alikuja akinguruma kama simba. Sijui ni nani alikuwa amemwambia niko hapo. Alinikaripia kwa maneno makali huku akinishutumu kwa kutolea watoto wangu kwa maadili yafaayo kisa mwanangu alikuwa amempiga na kumjeruhi mtoto wake walipokuwa wakicheza.  Muda wote nilikaa kimya kama maiti sikuongea neno lolote. Baada ya kuzomewa na wazee pale mangweni Mzee Kizingo aliondoka na hasira huku akinitishia kunionyeha yaliyomtoa nyoka pangoni.

 

Nilimaliza pombe yangu nikaondoka hadi kwangu nyumbani. Baada ya kuoga niliandaliwa mlo na bibi yangu. Kumaliza kula ilikuwa saa tatu usiku, niliaga watoto wangu wanane nikaingia chumbani kujilaza. Baada ya masaa matatu sikuwa nimepata usingizi, nilimtazama mama watoto nikamuona amezama kwenye usingizi wa pono huku akikoroma kama samaki.

 

Ghafla bin vuu nilisikia milio ya kutisha nje ya nyumba huku bati likigongwagongwa .Nilianza kutetemeka kwa woga nikajaribu kupiga nduru ila sauti haikutoka kwani nilikuwa nimefungwa sauti.  Mzee Kizingo alitokea kama kizuka na kusimama karibu na kitanda. Yani mzee Kizingo alikuwa mchawi ! Nilipigwa na butwaa. Kizingo aliongea maneno kadhaa niliyojua tafsiri yake kukatokea uteo mkubwa. Alinishika na kuniweka ndani ya uteo kisha akauamuru upotee, uteo ule ulipasua ukuta nikiwa ndani na kupaa angani. Nyuma nilisikia Kizingo akiongea maneno yaliyojirudia  kana kwamba anatumia vipaza sauti vya bunge la congress,’shiiikaa adaaaabu daaabu ya yaaaaa… aaaaaa aaaako!

 

Uteo ule ulipaa kama helikopta na kuolea baharini juu ya maji. Maji yalipojaa ulisukumwa hadi magomeni kisha ukapotea. Nakumbuka nikilia kama mtoto huku nikimtaja Kizingo anisamehe. Hadi hapo sijui nililala vipi hadi sasa ikiwa ni nimeamka mafungulia ng’ombe. Bandari niliyoamkia sikuwa  naijua hivyo ilibidi nisubiri kuanuke ndipo nitafute njia ya kuniregesha nyumbani. Nilitafuta magwanda kujiziba uchi  na kusubiri hatima ya kadhia hii.

 

 

RICHARD NGALA

(RICH BLAZE)

 

 

Use Facebook to Comment on this Post

Related Posts:

  • No Related Posts

About Richard Ngala

Check Also

Love can do it

Post Views = 2960 Before you begin to look for my hand, let me tell …

First dates

Post Views = 7917 I do realize that that my creative mojo isn’t back yet. …

One comment

  1. Kujiunga na majini wa Mombasa

Leave a Reply

Connect with:
Your email address will not be published. Required fields are marked *